Tuesday, 15 October 2013

HUYU NDIYE MWANAMKE ALIYEJITEKA NYARA...AMEKAMATWA HUKO NIGERIA


Polisi Kusini Mashariki mwa Nigeria, wamemkamata mwanamke mmoja aliyejidai kutekwa nyara kama njama ya kupata pesa kutoka kwa mumewe.

Nancy Chukwu anadaiwa kushirikiana na wanaume wengine kudai kuwa wamemteka nyara mjini Enugu na kisha kumshurutisha mumewe kulipa dola 780 za kimarekani kama kikombozi ili aachiliwe.

Lakini mumewe alikwenda kwa polisi ambao baadaye walimzuilia mkewe na washirika wake.

Utekaji nyara ni biashara maarufu sana Nigeria.

Jamaa za wanamichezo mashuhuri, kasisi na mamake waziri wa fedha, pamoja na wafanyakazi wengi katika viwanda vya mafuta wamewahi kutekwa nyara huku watekaji wao wakidai kikombozi kabla ya kuwaachilia.

Bi Chukwu, ambaye ni mfanyabiashara, alimpa mumewe nambari ya simu ya mtu aliyejidai kumteka nyara na mwanamume huyo baadaye alimpigia simu mumewe Chukwu na kumtaka kulipa pesa kwenye akaunti moja ikiwa alitaka kumuona mkewe hai tena.

Mwanamke huyo kumbe alikuwa amejificha na wanaume hao, akisubiri kupata habari njema kutoka kwa mumewe Marcus Chukwu za kulipa kikombozi hicho.

Lakini badala ya kulipa pesa hizo, mumewe mwanamke huyo alikwenda kwa polisi ambao waliweza kufuatilia nambari hiyo ya akaunti ambayo ilijulikana kuwa ya rafiki ya mtu aliyekuwa anajidai kuwa mtekaji nyara.

Bi Chukwu na washirika wake walikamatwa na msemaji wa polisi akasema kuwa baadaye walikiri kufanya uhalifu huo.

Mumewe mwanamke huyo alielezea kushutushwa sana na kuhusika kwa mkewe katika kashfa hiyo.

Hata hivyo haijulikani ikiwa kisa hiki kitakuwa mwisho wa ndoa kati ya wawili hao.
Source:bbcswahili.com

 

0 comments :

Post a Comment