Mfanyakazi wa zamani wa muda katika
Shirika la Usalama la Marekani, NSA, Edward Snowden, ambaye alifichua kuwepo
kwa mipango ya Marekani kufuatilia taarifa za mawasiliano ya watu, amesema
amefaniskisha lengo lake..endelea hapa chini..
"Kwa kuridhika binafsi, mpango
wangu tayari umefanikiwa," ameliambia gazeti la Washington Post.
"Tayari nimeshinda,"
amesema Bwana Snowden, ambaye ufichuaji wake mkubwa umesababisha Marekani
kuangalia upya sera yake ya ufuatiliaji wa taarifa za siri za watu na
mashirika.
Snowden mwenye umri wa miaka 30,
alifanya mahojiano na gazeti hilo nchini Urusi, ambako alipewa hifadhi ya
ukimbizi wa muda tarehe Mosi Agosti.
Bwana Snowden aliondoka Marekani
mwishoni mwa mwezi Mei, akichukua kiasi kikubwa cha nyaraka za siri kuhusu
mpango wa udukuzi wa Marekani.
Anakabiliwa na mashitaka ya ujasusi
nchini Marekani.
NSA iligundulika kuhusika katika
udukuzi wa data za simu. Taarifa za kina za watu na taasisi zilizolengwa na
udukuzi wa mashirika ya ujasusi ya Uingereza na Marekani zilichapishwa wiki
iliyopita na magazeti ya The Guardian, The New York Times na Der Spiegel.
Magazeti hayo yamesema orodha ya
watu na taasisi zipatazo 1,000 zilizolengwa ni pamoja na Kamishna wa Umoja wa
Ulaya, mashirika ya kibinadamu na maafisa wa Israel akiwemo waziri mkuu.
Makampuni makubwa ya teknolojia ya
mawasiliano nchini Marekani ya Google, Microsoft na Yahoo yanachukua hatua ya
kuzuia ukusanyaji wa data unaofanywa na serikali yao.
Mwezi Oktoba, habari ziliposambaa
kuwa NSA lilikuwa limedukua mazungumzo ya simu ya kiongozi wa Ujerumani
Chansela Angela Merkel, kulisababisha mvutano wa kidiplomasia kati ya Ujerumani
na Marekani.
Rais wa Brazil Dilma Rousseff naye
pia alikasirishwa na taarifa kwamba shirika la ujasusi la Marekani, NSA,
liliingilia mtandao wa kompyuta wa kampuni ya mafuta ya serikali ya Brazil,
Petrobras ili kukusanya taarifa na mawasiliano ya barua pepe na simu.
SOURCE:bbcswahili.com
0 comments :
Post a Comment